Select Page

MWANGI MAINA: Nafasi ya Kiswahili Afrika na Changamoto Zake

MWANGI MAINA: Nafasi ya Kiswahili Afrika na Changamoto Zake
  • KILELE cha maadhimisho ya pili ya Siku ya Kiswahili Duniani kimeshuhudiwa leo kote duniani
  • Kiswahili ni lugha ya kwanza ya Kiafrika kutunzwa na Umoja wa Mataifa. Ni mojawapo ya lugha rasmi za Umoja wa Afrika (AU).
  • Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC, imefanya sherehe za Kuadhimisha siku hii katika jiji kuu la Kampala, Uganda huku Waziri Mkuu wa Uganda Nabbanja Robinah akiongoza sherehe hizo .
Waziri Mkuu wa Uganda Nabbanja Robinah akiongoza maadhimisho ya siku ya Kiswahili Uganda | Picha: Jumuiya ya Afrika Mashariki

Leo ni Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani. Sherehe hiyo inaadhimishwa duniani kote kwa mara ya pili tangu UNESCO ilipoteua Julai 7 kuwa siku rasmi ya kuadhimisha lugha.

Na ingawa lugha hii inaleta umoja, sio watu wengi kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki wanaweza kuizungumza.

Kiswahili ni lugha ya Kibantu ya Waswahili wanaoishi kando ya pwani ya Bahari ya Hindi ya Afrika Mashariki. Idadi ya wazungumzaji wa Kiswahili, wawe wenyeji au wazungumzaji wa lugha ya pili, inakadiriwa kuwa milioni 200 kote duniani.

Kama mzungumzaji wa Kiswahili na raia wa jumuiya ya Afrika Mashariki, nilikumbana na kikwazo cha lugha nilipovuka Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mwezi Februari mwaka huu, na vile vile Uganda na Rwanda Mei 2022.

Utafiti wa kuibua ukweli jinsi Kiswahili kinavyozungumzwa kwa upana katika Afrika Mashariki kwanza ulinipeleka kwenye kisiwa cha marashi ya karafuu almaarufu Zanzibar.

Lugha hii inazungumzwa sana Kisiwani Zanzibar ingawa kwa ueledi kuliko vile tunazungumza katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi. Hata hivyo, Wakenya na Watanzania wanawasiliana kwa urahisi.

Nilizuru Kisiwa hiki mwezi Juni kwa mara ya tatu na ilikuwa rahisi kuwasiliana na wenyeji wa Zanzibar.

Mwangi Maina wakati wa likizo Zanzibar, Tanzania.

Mwezi Februari mwaka huu nilijipata Kinshasa wakati Papa wa Roma alikuwa akizuru mji huo kwa ziara yake ya kitume.

Mikoa mitano kati ya 11 ya Kongo ni ya wasemaji wa Kiswahili: Mkoa wa Orientale, Kivu Kaskazini na Kusini Mashariki, Maniema Mashariki ya kati, na Katanga Kusini magharibi.

Katika mji mkuu wa Kinshasa, wakongomani wanapata changamoto za kuzungumza Kiswahili kwa sababu ya kifaransa, lugha maarufu ambayo wakoloni wa Kibelgiji walitumia nchini Kongo. Vile vile kuna lugha ya lingala.

Lugha hii ina umaarufu mkubwa kutokana na muziki wa rhumba, ambao mara nyingi huimbwa kutumia lugha hiyo.

Dereva wangu alikuwa anazungumza Lingala na kifaransa pekee. Hatungeweza kuwasiliana kwa ufanisi isipokuwa kwa salamu za kifaransa ‘Bonjour na Bonsoir’ na wakati mwingine aliniambia ‘comsy-comsa’ maana yake sio nzuri wala mbaya.

Nchi hii ya Patrice Lumumba, mwanamapinduzi na shujaa, ni ya kuvutia sana. Mji mkuu wa Kinshasa una shughuli chungu nzima ingawa kuna msongamano wa magari na watu.

Nilifanya utalii katika mji huu, ambao uko kando ya mto Kongo mkabala na Brazzaville ambalo ni jiji kuu la nchi jirani ya Congo Brazzaville.

Majiji hayo mawili yapo umbali wa chini ya maili moja (1.6km), na kuifanya kuwa moja ya miji mikuu iliyo karibu zaidi duniani kama inavyoonekana kwa picha.

Watoto Brazzaville wanatazama ng'ambo ya mto Kongo hadi Kinshasa. Picha: Federico Scoppa/AFP/Getty

Watoto watatu wenye tabasamu na furaha walinilaki kwa nyimbo za jadi. Hata hivyo, hatungeweza kuwasiliana kwa sababu ya lugha. Walizungumza Lingala na Kifaransa.

Kabla ya kuzuru Kinshasa nilitembea nchi jirani ya Burundi Novemba 2022. Ilikuwa rahisi kuwasiliana na warundi katika mji wa Bujumbura. Wengi wa wakaazi wanaelewa na kuzungumza lugha ya kiswahili.

Wakati wa likizo Mei 2022 nilizuru Uganda na Rwanda.

Safari hii, ingawa ya kusisimua, ilithibitisha jinsi lugha inavyoweza kuzuia ushirikiano wa kikanda na biashara.

Ilikuwa safari ya barabarani ilioanzia jijini Nairobi kuelekea Kampala kupitia mpaka wa Busia.

Nimetumia njia hii hapo awali kwa hivyo ilikuwa rahisi sana kupenya.

Jambo la kupendeza ambalo nimeshuhudia ninapokuwa nikisafiri Uganda na ambalo singependa kukosa ni kula kuku wanaouzwa pembeni mwa msitu wa Mabira, kabla ya kufika Jinja.

Wachuuzi wanauza kuku wa kuchomwa, nyama ya mbuzi na ndizi za kiganda. Kwa Ush 1,000 (Ksh94), unapata kipande kikubwa cha kuku aliyechomwa vizuri.

Wachuuzi kwenye soko la Namawojjolo, Uganda.

Kuna mzaha unaosimuliwa hasa Tanzania: Kiswahili kilizaliwa Zanzibar, Kilikua Tanzania Bara, kikafa Kenya na kuzikwa Uganda.

Kiswahili kinaangaziwa kama lugha ya polisi na jeshi Uganda, hali ambayo zamani ilileta ugumu kwa lugha kukubalika na wananchi wengi kutokana na historia ya utawala wa kijeshi Uganda.

Rais Museveni amewarai Waafrika kuzungumza Kiswahili ili kusaidia katika uwiano wa bara hilo.

Lakini kuna matumaini mapya kwa wananchi. Sherehe za kuadhimisha siku ya Kiswahili duniani za ukanda wa Afrika Mashariki zimefanyika leo jijini Kampala.

Naibu Waziri Mkuu wa kwanza na Waziri wa Masuala ya Jumuiya, Rebecca Kadaga aliwataka wabunge wa Uganda kushiriki katika sherehe hizo.

“Kaulimbiu ya mwaka huu inadhihirisha kuwa kadri Kiswahili kinavyokua na kuenea duniani kote, kitaendelea kukutana na lugha nyingine ambazo zinaweza kuleta mafanikio kwa pamoja,” alisema Kadaga

Hata hivyo, ikiwa unataka kuelewa mji mkuu wa Uganda, kutoka Kampala ya kale ambako msikiti wa Gadaffi upo hadi kasri ya mfalme Kabaka huko Mengo, Kampala, usafiri wa bodaboda ndiyo njia bora zaidi.

Kwa bahati mbaya, mawasiliano ni shida kwa sababu wanabodaboda wengi hawaelewi Kiswahili.

Na kwa wale wanaokisema Kiswahili sio kwa ueledi sana. Mwendesha bodaboda wangu Kampala kabla ya kuondoka aliniambia kuwa watu Uganda wana mtazamo mkubwa kuhusu Kiswahili na wangetaka kukizungumza.

Mwangi Maina ni Mwandishi wa Habari aliyebobea katika Masuala ya Kanda na Diplomasia

 


Your support empowers us to deliver quality global journalism. Whether big or small, every contribution is valuable to our mission and readers.